Karibu Katika Tovuti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar

STAFF MAIL : Login

Awesome Logo

   

Kuhusu Mamlaka
Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) imeanzishwa chini ya kifungu cha 7 cha Sheria ya Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia nambari 6 ya mwaka 2016. Mamlaka hii imeanza kazi rasmi mwezi Machi 2017 kufuatia kuteuliwa kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka. Lengo la kuanzishwa Mamlaka hii ni kukuza, kusimamia na kudhibiti shughuli za Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia kwa eneo la Zanzibar kwa kuzingatia Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia nambari 6 ya mwaka 2016.
Dira
Kuwa mdhibiti bora wa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia inayochangia kukuza uchumi wa Zanzibar.
Dhamira
Kusimamia, kudhibiti na kukuza shughuli za Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa njia endelevu kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Zanzibar.
Misingi Mikuu
(a) Uadilifu na Usiri.
(b) Uwajibikaji na Uwazi.
(c) Taaluma.
(d) Usalama na Uendelevu.
(e) Ushirikishwaji wa jamii.
(f) Mashirikiano na Ubunifu.

Majukumu
Kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, majukumu ya ZPRA ni kama yafuatayo:
(a) Kufuatilia na kudhibiti shughuli za Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ikijumuisha makisio ya hifadhi na vipimo vya rasilimali zilizozalishwa.
(b) Kupitia na kuridhia shughuli ya utafiti iliyopendekezwa na kuwemo katika mpango kazi, mpango wa tathmini na makadirio ya Uzalishaji uliowasilishwa na Kampuni.
(c) Kupitia na kuidhinisha bajeti zilizo wasilishwa na Kampuni.
(d) Kutathmini mipango ya maendeleo na kutoa mapendekezo kwa Waziri kwa ajili ya kuidhinisha, kurekebishwa au kukataliwa.
(e) Kumshauri Waziri katika kutoa na kufuta leseni.
(f) Kutathmini hatua za mwisho za Uzalishaji, usitishaji, pamoja na ukomo wa shughuli za Mafuta na Gesi Asilia.
(g) Kuandaa ramani ya muongozo itakayoweza kupitiwa mara kwa mara inayoonesha maeneo yenye uwezekano wa Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
(h) Kushiriki upimaji wa Mafuta na Gesi Asilia na kuruhusu makisio na tathmini ya mrahaba na faida ya Mafuta au Gesi Asilia kwa maslahi ya nchi na itahusika kuidhinisha zoezi hilo.
(i) Kuhakiki gharama za Mafuta au Gesi Asilia za Kampuni.
(j) Kuhakikisha kwamba kampuni zinafuata sheria, kanuni, taratibu na masharti ya mkataba.
(k) Kufanya au kuwezesha kufanyika utafiti wa awali na kutathmini maeneo muhimu ya Mafuta na Gesi Asilia.
(l) Kusimamia mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia.
(m) Kuhakikisha uvunaji wa hali ya juu wa raslimali za Mafuta na Gesi Asilia.
(n) Kuendeleza mipango mizuri inayotekelezeka kwa gharama nafuu.
(o) Kuhakikisha matumizi mazuri ya miundo mbinu iliyopo na iliyopangwa.
(p) Kuhakikisha uanzishwaji wa Kituo Kikuu cha Mfumo wa Taarifa kwa watu wanaohusika na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia, kusimamia taarifa za Mafuta na Gesi Asilia na kutoa taarifa na machapisho ya kila siku kuhusu shughuli za Mafuta na Gesi Asilia.
(q) Kuchukua hatua za ulazima kutekeleza matakwa ya leseni au kanuni zozote na kulinda afya na usalama wa wafanyakazi na jamii.
(r) Kuhakikisha na kuwezesha ushindani, upatikanaji na matumizi ya miundombinu kwa wengine.
(s) Kufuatilia masharti ya waendeshaji na shughuli zao za kibiashara kwa kuhakikisha kwamba ushindani na haki inalindwa.
(t) Kuhakikisha washiriki wanafuata Sheria hii na kutoa adhabu kwa wanaopinga au wanaovunja kanuni, amri, taratibu au masharti ya mkataba.
(u) Kufanya mambo mengine yote ambayo ni muhimu, ya kuharakisha au ambayo ni muafaka ili kufikia malengo ya Sheria hii.

Miradi
(a) Utafutaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia kwa kitalu cha Pemba-Zanzibar.
(b) Uanzishwaji wa kituo kikuu cha kuhifadhia Taarifa za Mafuta na Gesi Asilia.
(c) Usafishaji wa Taarifa za zamani za mtetemo kwa eneo la kina kirefu cha maji, eneo la mashariki mwa Zanzibar.
Muundo
ZPRA imeundwa na Idara 6 ambazo zimegawika katika jumla ya Divisheni 11 kama zinavyoonekana hapo chini: -
1. Idara ya Utafutaji, Uzalishaji na Uchambuzi wa Kiuchumi.
Divisheni ya Utafutaji, Uchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi na Taratibu za Utoaji Leseni.
Divisheni ya Uendelezaji na Uzalishaji.
2. Idara ya Usimamizi wa Taarifa.
Divisheni ya Usimamizi wa Taarifa za Utafutaji na Uzalishaji.
Divisheni ya Usalama wa Taarifa.
3. Idara ya Afya, Usalama na Mazingira.
Divisheni ya Afya na Usalama.
Divisheni ya Mazingira.
4. Idara ya Sheria na Matekelezo.
Divisheni ya Uratibu wa Shughuli za Bodi ya Mamlaka na Masuala ya Kesi.
Divisheni ya Usimamizi wa Mikataba na Matekelezo.
5. Idara ya Mipango, Fedha na Utawala.
Divisheni ya Mipango na Tafiti.
Divisheni ya Utawala na Rasilimali Watu.
Divisheni ya Fedha.
6. Ofisi ya Pemba.

ZPRA ina vitengo 4 vinavyojitegemea ambavyo ni: -
(a) Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.
(b) Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
(c) Kitengo cha Manunuzi na Uondoaji wa Mali chakavu.
(d) Kitengo cha Mahusiano ya Umma.
Maelezo zaidi

Choose Your Color
You can easily change and switch the colors.