Karibu Katika Tovuti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar

STAFF MAIL : Login

Awesome Logo

Mnamo mwaka 2016 Baraza la Wawakilishi Zanzibar liliandika historia mpya ya Zanzibar baada ya kupitisha Sheria Nambari 6 ya Mwaka 2016 Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar. Sheria hii inayosimamia na kutoa miongozo ya utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia pamoja na mambo mengine imeanzisha taasisi muhimu katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ikiwemo Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.

Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar
imeanzishwa mnamo June 2018 ambayo imeanzishwa chini ya kifungu cha 32 cha Sheria Nambari 6 ya Mwaka 2016 ya Mafuta na Gesi Asilia na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Nambari 15 ya Mwaka 2013.

Majukumu
Majukumu ya ZPDC yameelezwa chini ya kifungu cha 32 cha Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar ya Mwaka 2016 pamoja na kifungu cha 3 cha Katiba ya Kampuni (Memorandum and Articles of Association).
Miongoni mwa majukumu hayo ni:-
a. Kushiriki katika shughuli za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa niaba ya Serikali.
b. Kuwa chombo cha biashara pamoja na kulinda maslahi ya Taifa katika biashara ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.
c. Kusimamia masuala ya biashara na kiufundi katika masuala ya utafutaji na uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa niaba ya Serikali.
d. Kuingia ubia na Kampuni za Kimataifa katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.

Dhamira
Kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni chombo cha Serikali chenye kulinda maslahi ya Taifa katika hatua zote za sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Misingi Mikuu
Usalama: Kuhakikisha usalama wa kiwango cha juu katika shughuli za Kampuni.
Uwazi: Utekelezaji wa shughuli za Kampuni katika hali ya uwazi.
Uadilifu: Utekelezaji wa kazi za Kampuni kwa uaminifu, kimaadili na kimalengo.
Utaalamu: Utekelezaji wa kazi kwa umahiri na utaalamu.
Ufanisi: Utekelezaji wa kazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kuhakikisha matumizi bora ya Rasilimali.

Mafanikio ya Kampuni tokea kuanzishwa kwake.
a) Kusaini Mkataba wa Mgawanyo wa Mapato (Production Sharing Agreement) yanayotokana na Mafuta na Gesi Asilia na Kampuni ya RAKGas kutoka Ras Al Khaimah kwa Kitalu cha Pemba - Zanzibar.
b) Kuandaa Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa Miaka mitano 2019-2023. Mkakati huu unaelezea mipango ya Kampuni katika ushiriki wake kwenye utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
c) Kuandaa Kanuni na miongozo ya utendaji wa Kampuni (Miongozo yaUajiri, Kanuni za Usimamizi wa Fedha na Kanuni za Watendaji).
d) Kusaini Hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambao utaleta mafanikio katika kubadilishana maarifa, ujuzi na uzoefu katika sekta hii ya mafuta na Gesi Asilia.

Maendeleo ya Utafiti
Mnamo Oktoba 2017 hadi February 2019 kabla ya kuanzishwa kwa ZPDC, utafiti wa mafuta na gesi asilia ulifanyika kwa zoezi la mtetemo (2D Seismic Survey) ambapo Shughuli iliyofanywa ilijumuisha uchukuaji wa taarifa kutoka baharini, nchi kavu na katika kina kifupi cha bahari.
Utafiti huu ulifanywa na Kampuni ya Bureau Geophysical Prospecting (BGP) kutoka Jamhuri ya watu wa China chini ya usimamizi wa wataalamu wazalendo kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA).
Kwa upande wa bahari, zoezi lilifanywa kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 2,815.6, likijumuisha jumla ya mistari 66. Kwa upande wa nchi kavu, uchukuaji kwa njia ya mtetemo, ulifanywa katika jumla ya mistari 25 yenye urefu wa kilomita 717.1. Kadhalika, katika maeneo ya kina kifupi cha maji, zoezi lilifanywa kwenye mistari 10 yenye urefu wa kilomita 244.
Matokeo ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya Anga (Full Tensor Gradiometric Survey) na Mtetemo (2D Seismic Survey) yameonesha uwezekano mkubwa wa kuwepo miamba yenye uwezo wa kuhifadhi Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba – Zanzibar.
Hii ni kwa sababu, matokeo ya taarifa zote yameonesha kuwepo kwa viashiria vyote vya mfumo wa uhifadhi wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia (Petroleum System Elements (PSE).
Kwa upande wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya mitetemo, matokeo yameonesha kwamba yapo maeneo matano (5) yenye uwezekano wa kuwepo na rasilimali ya gesi asilia katika Kitalu cha Pemba – Zanzibar.
Sehemu zenyewe ni eneo la bahari liliopo baina ya Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Unguja na Kusini mwa kisiwa cha Pemba, eneo la Kaskazini, Kusini na Mashariki mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Pemba na eneo la Kusini mwa Kisiwa cha Pemba.
Baada ya utafiti huo hatua inayofata ni kuzifanyia usafirishaji wa mara ya pili taarifa zilizoonekana kutokuwa na ubora wa kuridhisha katika zoezi la mtetemo lililokamilika.
Pia kuendelea na utafutaji rasilimali hizi katika kina kifupi kwa njia ya mtetemo kwenye maeneo maalum yaliyogundulika kuwa na viashiria vya kuwepo kwa mafuta na gesi asili.
Sambamba na hilo kutambua eneo la kuchimba kisima cha utafutaji (Identification of well location) pamoja na kuanza kazi ya kuchimba kisima cha kwanza cha utafutaji (Exploration Well Drilling) ambazo zote hizo zinatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Maelezo zaidi

Choose Your Color
You can easily change and switch the colors.