Ugawaji wa Vifaa vya Mwani kwa vikundi 125 Mkoa wa Kaskazini Pemba

  • Mwanzo
  • News
  • Ugawaji wa Vifaa vya Mwani kwa vikundi 125 Mkoa wa Kaskazini Pemba

Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika kuwaendeleza wananchi kiuchumi kupitia miradi ya uchumi wa buluu, hususan sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani, ili kuhakikisha wananchi wanaongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Khatib Juma Mjaja, aliyasema hayo wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya kilimo cha mwani kwa vikundi 125 vya shehia 14 vya wakulima wa mwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Pemba.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, imeweka kipaumbele katika kuwawezesha wananchi kupitia miradi ya kiuchumi inayotokana na rasilimali za bahari.

“Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya uchumi wa buluu na sekta ya uvuvi ili kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya kuwafikia wananchi wa chini,” alisema Mjaja.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alisema Serikali imeona umuhimu mkubwa wa kuimarisha zao la mwani, hivyo ikaamua kugawa vifaa na zana mbalimbali kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hiyo.

“Zao la mwani ni miongoni mwa mazao muhimu yanayoliingizia taifa pato na kutumika katika nchi mbalimbali duniani. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalilea na kulienzi zao hili,” alisisitiza.

Mjaja aliwataka wakulima hao kuhakikisha wanavitunza vifaa walivyopatiwa ili viweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu, sambamba na kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji.

“Nawaomba mtunze vifaa hivi vizuri, vitawasaidia kwa muda mrefu na vitaboresha uzalishaji wenu. Tuwe walinzi wa rasilimali zetu,” alisema Mjaja.

Sambamba na hayo alitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wakuu wa kitaifa — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi  kwa jitihada wanazoendelea kuzichukua katika kuwaendeleza wananchi kupitia miradi ya maendeleo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi,Captain Hamad Bakar Hamad, alisema serikali ya Zanzibar inatekeleza ahadi tatu zilizotolewa na Rais Dk. Mwinyi kwa wakulima wa mwani, ikiwemo kutoa elimu ya kilimo cha uzalishaji mwani, kuwasambazia zana za kisasa, na kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika.

“Zaidi ya asilimia 90 ya boti za mwani zimepelekwa Pemba, na serikali imeanzisha kampuni ya mwani ili kuhakikisha soko la uhakika kwa wakulima wetu,” alisema.

Alifahamisha kuwa kiwanda cha mwani kilichopo Chamanangwe kinaendelea kununua mwani mbichi na mkavu kutoka kwa wakulima, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo na kukuza mapato ya wakulima.

“Tumeanza pia mradi wa kuwapatia wakulima mashine za kusaga mwani na vifaa vya kuongeza thamani, ili wakulima waweze kuzalisha bidhaa zinazotokana na mwani,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Salum Moh’d Hamza, alisema Wilaya ya Micheweni inaongoza kwa uzalishaji wa mwani, ikiwa na vikundi 125 vilivyosajiliwa.

Alifahamisha kuwa wizara itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo kuhakikisha wakulima wanapata mafunzo na msaada wa kiufundi katika kuongeza uzalishaji.

Naye, Amina Ussi Khamis, Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi inayodhaminiwa na Shirika la Kimataifa la IFAD, alisema ugawaji huo wa vifaa ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wa kuwasaidia wakulima wa mwani nchini.

“Kwa upande wa Zanzibar, jumla ya vikundi 350 vya wakulima wa mwani vimenufaika na mpango huu, ambapo 270 vipo Pemba na 80 Unguja,” alisema Amina.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa mwani, Rashid Omar Matar, aliishukuru serikali kwa kuwaendeleza na kuwatimizia ahadi walizopewa na viongozi.

“Tunampongeza sana Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza ahadi zake. Vifaa hivi vitatusaidia sana kuongeza tija na kuboresha maisha yetu,” alisema.

 

Naye Kaije Said Bakar kutoka Tumbe – Pemba, alitoa shukrani kwa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi kwa kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Shirika la IFAD kuwapatia vifaa hivyo, akisema hatua hiyo imeleta matumaini makubwa kwa wanawake wakulima.

“Tunashukuru sana kwa vifaa hivi. Tutavitunza na kuvihudumia ili vitusaidie kwa muda mrefu,” alisema.

Categories

At vero eos et accusamus et iusto odio digni goikussimos ducimus qui to bonfo blanditiis praese. Ntium voluum deleniti atque.

Melbourne, Australia
(Sat - Thursday)
(10am - 05 pm)
Shopping Cart (0 items)
Translate »