BIASHARA NA MIUNDOMBINU YA BAHARI
Zanzibar imebarikiwa na fursa mbali mbali za uimarishaji wa Sekta ya Usafiri wa Baharini pamoja na mifumo yake ya kibiashara, huduma na miundombinu. Lakini bandari chache, miundombinu isiyotosha ya bandari ikiwa ni pamoja na ufinyu wa eneo la kushusha na kupakia mizigo kwa ajili ya usafirishaji wa baharini na uvuvi, ufanisi mdogo wa bandari, n.k ni mambo yanayokwamisha utekelezaji wa kasi wa ajenda ya Uchumi wa Buluu nchini.
VIPAUMBELE
Kwa kuliangalia hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka vipaumbele vifuatayo vya Uchumi wa Buluu katika Sekta hii:
Kutumia njia ya uwekezaji ya ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi ili kujenga bandari mpya za abiria, mizigo na uvuvi, na kuboresha ufanisi wa miundombinu na huduma za bandari zilizopo
Kukuza tafiti za tathmini ili kutambua, kurasimisha, kubadilisha na kuziendeleza bandari zisizo rasmi na madiko kwa utambuzi rasmi
Kujenga na kusimamia vituo vya kutoa huduma baharini
Kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa vyombo vya baharini katika maji ya ndani ya Zanzibar ili kuhakikisha kuwepo kwa mawasiliano ya kutosha kati ya wasimamizi wa mienendo ya vyombo vya baharini na manahodha
Kuhakikisha kuwepo kwa mfumo mzuri wa kusimamia utekelezaji wa sheria za bahari
Kukuza usambazaji wa teknolojia ili kukuza uwezo wa miundombinu ya sekta za bahari kwa kushirikiano na washirika wa maendeleo na wadau muhimu katika mfumo wa msaada wa kiufundi, kubadilishana taarifa na mafunzo
Kukuza utayari wa bandari katika ushindani wa usajili wa meli kimataifa
Kuwezesha na kukuza uwekezaji katika viwanda vya kusindika bidhaa za Uchumi wa Buluu
Kukuza uanzishwaji na uwekezaji wa viwanda vinavyohusiana na shughuli za kiuchumi na huduma za baharini
Kuanzisha bandari huru na maeneo kwa ajili ya huduma za usafirishaji bidhaa za mpito ili kuimarisha uongozi wenye kuleta ubunifu katika usafirishaji na huduma baharini
Kujenga mashirikiano na mashirika ya usafirishaji ili kuongeza uwezo wa kusafirisha bidhaa nje ya nchi kupitia baharini



